MABINGWA wa Bara, Simba SC wanatarajiwa kuondoka leo Dar es
Salaam kwenda Oman kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa na Ligi Kuu pamoja na
Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kuhusu Kombe la Mapinduzi, Simba imegawa vikosi viwili na
kile ambacho kilichukua Kombe la Sup8R Banc ABC kwa kuzifunga Azam FC na Mtibwa
Sugar ndicho kitabaki kwenye Kombe la Mapinduzi chini ya kocha Jamhuri Kihwelo
‘Julio’ na Mganda Richard Hamatre.
Kikosi hicho cha Mapinduzi kina wakali kama Ramadhan Singano
‘Messi’, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo, Hassan Isihaka,
Hassan Hatibu, Miraj Adam na wengine ambao wote wanachezea Simba A.
Wachezaji wanaobaki kwenye Kombe la Mapinduzi, watakwenda
Oman baada ya mashindano hayo pamoja na kocha Julio.
Simba SC kesho inatarajiwa kumenyana na Azam FC katika Nusu
Fainali ya Kombe la Mapinduzi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mchezo huo utakuwa ni marudio ya Nusu Fainali ya mwaka jana,
ambayo Azam FC waliitoa Simba SC kwa kuichapa mabao 2-1.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Muingereza Kalimangonga Sam
Daniel Ongala, maarufu kama Kali, amesema kwamba wamefurahia kukutana na Simba
SC katika Nusu Fainali kuliko Tusker ya Kenya, kwa sababu hiyo itakuwa njia ya
mkato kwao kuingia Fainali.
Ikiwa Oman, Simba itakaa kwa wiki mbili na itacheza mechi
tatu za kujipima nguvu dhidi ya timu ambazo wameandaliwa na wenyeji wao Fanja
FC. Aidha, wameandaliwa makocha watatu huko, wakiongozwa na beki wa zamani wa
Simba SC, Talib Hilal kuungana na makocha wa Simba kuinoa klabu hiyo ikiwa
nchini humo.
Hiyo ni ziara ya mafunzo, ambayo lengo lake ni kuiweka sawa
Simba SC kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Ligi ya
Mabingwa Afrika.

Post a Comment